Thursday, 1 October 2015

TUNAWAANDAAJE WATOTO WANAPOFIKIA UMRI WA KUBALEHE

TUNAWAANDAAJE WATOTO WANAPOFIKIA UMRI WA KUBALEHE
Na Ferdinand Shayo,Arusha.
 
Wazazi wengi wamekua wakikaa kimya na kuona aibu kuzungumza na watoto wao juu ya mabadiliko ya miili yao inayotokea pindi wanapobalehe na namna ya kuweza kukabiliana na mabadiliko hayo kabla ya kuingia kwenye hatari.

Ukimya ambao haujengi unaharibu ,ukimya wa kutokuchukua hatua na kuacha mambo yajiendee yenyewe .
Watoto wetu wanaangamia kwasababu ya ukimya wetu ,wanakosa mafunzo ya kutosha juu ya hatua wanayoipitia,mihemko ya mwili,misukumo ya makundi rika,kuwakwa kwa tama za mwili isivyo kawaida.
Hatua wanazopitia watoto tayari wazazi wao walishazipitia hivyo wazazi wana uzoefu mkubwa wa hiki kipindi cha kubalehe kwakuwa walishakipitia lakini ni wazazi wangapi wanawashirikisha watoto wao jinsi walivyopita kipindi cha kubalehe.
“Wazazi wengi wameweka kumbukumbu zao za kubalehe kwao wenyewe bila kuwashirikisha watoto wao na kuwaacha watoto wao wakiingia kwenye matatizo yale yale ambayo waliyoingia pindi walipobalehe.
Wanawaacha watoto wao bila kuwapa tahadhari ,mafunzo ya kuzungumza nao juu ya kipindi wanachopitia na jinsi ya kupita salama.
Watoto ambao hawakupita salama kwenye hiki kipindi maisha yao yalianza kuharibika katika kipindi hiki,ndoto zao zikapeperuka na matarajio yao yakayeyuka.
Kipindi cha kubalehe ni mtihani kwa watoto na wengi wamefeli katika umri huo wametumbukia katika mahusiano ya ngono wakiwa katika umri mdogo,wengine wakipata mimba na kuacha masomo huku wengine wakiambukizwa Virusi vya UKIMWI,kujiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya.
Maisha yanafananishwa na mpira wa miguu ambapo mchezaji anatakiwa kuandaliwa vyema kupewa mbinu za kushambulia,kujilinda dhidi ya adui kabla ya kuingia kwenye mchezo ili aweze kushinda atakapoingia mchezoni.
Ni ngumu kumfundisha mchezaji akiwa tayari mchezoni ,uwanjani kama Kocha ama Mzazi unapaswa kumfundisha mtoto wako kabla hajaingia katika umri huo ambao ni hatua nyingine ya maisha na mabadiliko makubwa ya mwili wake yanatokea.
Watoto wengine wanapofikia umri huo wamekua hawajui juu ya mabadiliko yanayotokea kwenye miili yao wengine wanaogopa ,hali hiyo inawapa wasi wasi na kutokujiamini.
Kuna mjadala ulizuka nchini Kenya baada ya kuona vitendo vya Wanafunzi wengi kupata mimba wakiwa katika umri mdogo na wengine kulazimika kuacha masomo ,waligundua kuwa watoto wanashiriki vitendo vya ngono wakiwa bado wadogo hasa umri wa kubalehe.
Katika mjadala huo wako waliokuja na mapendekezo mengi ikiwemo kuwapatia watoto waliobalehe Kondom na vizibiti mimba ili waweze kujikinga na mimba na maambukizi ya Magonjwa ya zinaa ikiwemo UKIMWI.
Wako walioonyesha kuunga mkono suala hilo na wengine kupinga suala hilo ,huku wakitoa sababu ya kuwakinga mabinti na mimba za utotoni zinazokatiza masomo yao.
Mzazi mmoja alipinga vikali watoto kupewa kondom na vidhibiti mimba na kupendekeza kuwa elimu itolewe kwa watoto ambayo itakuwa kinga kamilina sio vifaa hivyo.
Elimu zaidi itolewe juu ya kukabiliana na mabadiliko ya mwili,umri sahihi na wakati sahihi wa kujihusisha na mahusiano ya ngono.
Bado wazazi wako kimya kuwaelimisha watoto wao kuhusu masuala ya jinsia wengine wanadai kuwa watajifunza shuleni.
Mfumo uliko mashuleni hauwawezeshi watoto kujifunza juu ya miili yao na kuitawala wanajikuta wanatumbukia kwenye matatizo katika umri wa kubalehe.
Mashuleni watoto wanafundishwa bailojia hawafundishwi elimu ya jinsia itakayowasaidia kupata taarifa sahihi juu ya mabadiliko ya miili yao,kujitawala,kujiongoza na kujisimamia na umri sahihi wa kuingia kwenye mahusiano.
Wakati umefika sasa kwa wazazi kuvunja ukimya na kuamua kuzungumza na watoto wao ili kuwanusuru na hatari zilizoko mbele yao.
Wazazi wamekua kimya wameiacha dunia iwafundishe watoto wao na inawafunza kweli kweli inawafunza hata vile ambavyo hawakutaka kujifunza.
Haitoshi kusema kuwa watoto wenyewe wanaona hali halisi iliyopo kwenye mazingira na dunia wakajifunza,Wanahitaji elimu ya kukabiliana na mazingirahatarishi ili wasibadilishwe na mazingira badala yake wayabadadilishe mazingira,wasibadilishwe na dunia bali waibadilishe dunia.
Wasibadilishwe na makundi rika yanayowazunguka (peer pressure) kwa kuwa wana msingi imara uliojengwa na wazazi.
Katika dunia ya sasa mambo mengi yameharibika japo si yote tunapokaa kimya bila kuchukua hatua yoyote na si tuna makosa makubwa kuliko ya wale wanaoharibu.
Inawezekana chukua hatua sasa
ferdinandshayo@gmail.com
0765938008

No comments:

Post a Comment