Saturday 3 October 2015

Badili maisha kupitia fikra zako

by Robison Sisyan | Makala

 
WATAALAMU wa masuala ya saikologia wanasema zaidi ya asilimia 95 ya maisha yetu ni matokeo ya fikra zilizopo ndani yetu na asilimia 5 ni mazingira yanayotunguka na vitu vingine.



Kutokana na utafiti huu unatufanya tuamini kuwa unaweza kubadilisha maisha yako kupitia fikra zako.
Ila kuna changomoto kubwa katika hili, watu wengi hawaamini kwamba wanaweza kubadilisha maisha yao kupitia fikra zao. Wanahisi ni njia rahisi na huku wao wakiamini kuwa mafanikio ni kitu kigumu.

Ni kweli kwamba ni njia rahisi na tunavyoamini kuwa maisha ni magumu ni kweli yanakuwa magumu kwani huo ndio ukweli tunaoujua, lakini nakushauri tumia njia rahisi ya kubadilisha maisha yako kupitia fikra zako.

Sisi ni matokeo ya fikra zilizokomaa katika akili zetu na kutengeneza ukweli wa maisha tulionao sasa, kupitia fikra zetu tumepewa uwezo wa kujitengenezea bahati zetu wenyewe.

Bahati hutokea pale maandalizi yanapokutana na fursa kama huna maandalizi kila siku fursa zitakuwa zinapita mbele yako na utashindwa kuzitambua, na wale wenye maandalizi watakutana nazo na kujitengenezea bahati zao.

Matokeo ya fikra zetu ni makubwa kuliko tunavyodhani. Wote tumezaliwa tukiwa hatuna uwoga wala kusitasita, lakini vyote hivi vinatukuta katika malezi na watu wanaotuzunguka, pale tunapoanza kukosolewa na kuadhibiwa tunapokosea.

Hapo ndipo fikra za uwoga na kutokujiamini zinaanza kukua katika maisha yetu mpaka tunakuwa watu wazima.

Kwa kupitia malezi ya aina hiyo tumekuwa waoga kujaribu kwa kuogopa kufeli kwa sababu tulishaambiwa hutakiwa kukosea hata shuleni pia ukikosea unaadhibiwa. Kwa hofu hiyo inakufanya kushindwa kuwa wabunifu na watekezeji katika maisha yetu ya kila siku.

Kupitia fikra zetu tumejijengea uwezo wa kuamini vitu tunavyohisi tunaweza na vile ambavyo tunahisi haviwezekani.

Ni ukweli usiopingika kwamba kila mtu katika akili yake kutokana na mazingira uliyopo, elimu yako, historia ya ukoo wenu, hali ya uchumi uliyonayo unahisi kuna mambo huwezi kufanya.

Hivi ni vizuizi tulivyojiwekea katika akili zetu kupitia fikra zetu na kuona kuna mambo hatuwezi kuyafanya au kubadilisha hali fulani katika maisha yako.

Hiyo mipaka uliyojiwekea ndiyo imekufanya uwe hapo ulipo na kushindwa kuchukua hatua madhubuti za kubadilisha maisha yako.

Watu wengi tunafanya mambo chini ya kiwango au katika uwezo wetu. Tumekuwa watu wa kuwaza bila kuweka katika matendo fikra zetu, tukiogopa kushindwa.

Kupitia fikra pia unajitambua wewe ni nani? Hivyo ukijitambua vibaya, huwezi ukafanya vizuri, au ukitasfiri katika upande hasi wa kuwa huwezi, kamwe hutaweza.

Watu wengi waliofanikiwa hawakusubiri serikali iwawekee miundombinu na hawakusubiri wapate mitaji mikubwa.

Mfano jiulize unalalamika kuwa hali ya uchumi ni ngumu, lakini angalia kuna biashara ngapi zinakuwa kwa kasi na watu wanatengeneza pesa kila uchao. Hivyo tatizo sio hali ya nchi, bali tatizo ni wewe kupitia fikra zako.

Kupitia fikra zetu tunatengeneza maisha yetu ya baadae, vitu havitokei kwa bahati mbaya, vyote vinakuwa vimepangwa.

Kwa kufikiri kimkakati ni vema ukatambua siri iliyopo kwenye kuandika kile unachokifikiri, kuna nguvu kubwa ya kuandika mawazo yako, kupitia kuandika ndiko kunafanya uone mawazo yako katika uhalisia na inakupa nguvu ya kuona unaweza kuyatekeza.

Bila ya kuandika, mawazo mengi mazuri yatakuwa yanapita katika akili yako kama hujazoe kuyatambua utaona kama ndoto za mchana na kuyaacha yapite.

Usiogope na kuanza na mwanzo mdogo, hakuna anayeanzia juu. Wote waananza katika hali ya kawaida, lakini wanamaliza kama mashujaa, na wewe usiogope kuanza hata kama hali iko vipi, bila kuchukua hatua utabaki hapo hapo. Anza sasa kubadilisha maisha yako kupitia upeo wako mkubwa wa kufikiri bila woga wala hofu.

Kupitia wewe uwe chachu ya madiliko pale ulipo, hakuna mtu wa kuja kuweka sawa hali yako kiuchumi, katika familia yako ila wewe.


Usimuangalie mtu mwingine ila wewe hasa ndio unatakiwa kuweka hali hiyo sawa.

No comments:

Post a Comment