Thursday, 8 October 2015

NIDHAMU YA FEDHA NGUZO YA MAFANIKIO YA KIUCHUMI



NIDHAMU YA FEDHA NGUZO YA MAFANIKIO YA KIUCHUMI

Na Ferdinand Shayo,Arusha.
Ili kuyafikia mafanikio ya uchumi nidhamu ya fedha ni ngazi inayoweza kukupandisha juu katika kiwango kingine cha mafanikio na kuyafikia malengo  uliyojiwekea.
Umewahi kuona watu wanafanya kazi katika kampuni moja wanalipwa mshahara unaofanana lakini mafanikio yao hayajafanana ,mmoja amejenga nyumba ya kuishi mwingine kapangisha,mmoja ana miradi yake nje ya kazi mwingine anasubiri mwisho wa mwezi ufike ili aweze kupata mshahara kwake yeye bila mshahara hakuna maisha.
Nini kinawatofautisha watu hawa wakati wanalipwa stahiki zinazofanana kubwa linaloonekana hapa ni nidhamu ya fedha  na kutimiza malengo kunapelekea kuwe na pengo kubwa la kiuchumi hata kama mishahara iko sawa.
Ili kujenga uchumi imara unaofanana na nyumba nzuri na imara unahitaji kuwa na nguzo nne,nguzo mojawapo ni nidhamu ya fedha,nguzo ya pili ni kufanya kazi kwa bidii na kujituma ,nguzo ya tatu kutoa huduma au bidhaa bora kwa wateja,nguzo ya nne ni upekee na ubunifu ambao unakusaidia kushinda na kuhimili ushindani katika soko.
Nguzo hizi nne zinafanya uchumi wako kuwa imara na usiotikisika kirahisi siku ya leo tutazungumzia nguzo moja ya nidhamu ya fedha.
Umewahi kuona mtu anafanya biashara ya kuuza mboga mboga sokoni mchicha,sukuma ,mnafu na kadhalika na mwingine ameajiriwa katika taasisi kubwa ama serikalini,huyu anayeuza mboga amejenga nyumba anasomesha watoto lakini huyu aliyeajiriwa hana nyumba,kapangisha ,haishi kulalama na mikopo imemuandama.
Jiulize nini kinatokea kwa huyu muuza mboga na muajiriwa wakati muajiriwa amemzidi kipato lakini hali ya maisha yao inatofauitiana ,ukitazama kwa jicho la tatu utagundua kuwa nidhamu ya fedha inahusika kuamua mtu awe na hali gani ya maisha,afanikishe malengo kwa kiwango gani.
Bila nidhamu ya fedha ni vigumu kufanikiwa kimaisha watu wengi wameshindwa kusanga mbele kiuchumi,kukua kiuchumi wakadumaa kwa sababu tu ya kukosa nidhamu hiyo ,maisha yao yamekua vile vile miaka nenda rudi hakuna kilichoongezeka na wengine kujiona kama wamelogwa pasipokujua tatizo ni wao wenyewe.
Siri ya mafanikio ipo kwenye jinsi unavyotumia kila fedha inayopita mikononi mwako kunaweza kukufanya ukawa tajiri au masikini.Jichunguze fedha unayoipata unaitumiaje ? unaweka akiba? Unawekeza ili iongezeke? Una mpangilio mzuri wa fedha zako?
Watu wengine wakipata fedha wanazitumia zikikaribia kuisha wanakumbuka  mipango yao baadae ile hali pesa iliyoko haitoshi hata kuanza,hawaelekezi pesa kwenye malengo na mipango waliyojiwekea,wanakosa vipaumbele na kujikuta hawapigi hatua mbele wanazidi kurudi nyuma.
Wengine huishia kufanya matanuzi,anasa ,nguo za bei ghali na kufanya mambo ya kujionesha bila kujali wanaathirika vipi kiuchumi ile hali uchumi wao bado ni mchanga hujakomaa kiasi cha kuwazalia matunda ambayo wanaweza kuyatumia bila kuathiri mitaji yao.
Nidhamu ya fedha imesababisha watu wengi kufilisika na kuwa omba omba kwenda kukopa kwenye taasisi za fedha huko nako wanajikuta wanashindwa kurejesha kwasababu ukishindwa kuwa na nidhamu kwenye fedha zako huwezi kuheshimu fedha za mwenzako.
Watu wengi wanatumia fedha zao kununua minyoo ya uchumi vitu ambavyo vinawadhoofisha kiuchumi badala ya kuwaimarisha kiuchumi kama vile simu za bei ghali ,gari la kutembelea linakula mafuta service huna biashara yoyote afadhali hata lingekua la biashara likiondoka asubuhi jioni linakuletea mahesabu.
Bado utumwa wa maisha ya kujionyesha unawatesa watanzania wengi mtu anataka watu wamuone kuwa yeye ndo yeye,awakomeshe,awafunge midomo ,kutaka kuzua gumzo mitaani na kwenye kumbi za starehe,waswahili wanasema kuweka heshima bar.
Wamesahau kuwa heshima ya mtu inakuja pale anapotimiza malengo na mipango yake,kujiweza kiuchumi na kuisaidia jamii inayokuzunguka.
Tatizo la matumizi mabaya ya fedha lilianzia kwenye familia wazazi baba na mama watoto wakaiga likakua na kuwa tatizo la kitaifa sasa.
Familiani shule ya kwanza inayofundisha juu ya fedha ,nidhamu ya fedha baadae shule zinafundisha,Wazazi hawana budi kuwafundisha watoto wao kuwa na nidhamu ya fedha ili waweze kufanikiwa kiuchumi.
Jiulize ni nini kinamfanya tajiri kuwa tajiri na pia ni nini kinamfanya masikini kuwa masikini ? yako mengi ya kujifunza kama unataka kubadilisha hali yako ya kiuchumi na kuondokana na umasikini ambao ni tatizo sugu linaloweza kuondolewa na dhamira ya mtu mmoja mmoja kwa kuamua tu na sio kuongea tu?
Ifike mahali tujifunze kuwa na mpangilio ulio bora wa matumizi ya kila shilingi inayopita katika mikono yetu iwe ndogo au kubwa kwani maamuzi tunayofanya juu ya fedha zetu ndio yanatufanya tuwe matajiri au masikini.
Kama ndivyo tuanze kujifunza kuweka akiba,kuwekeza,kununua hisa katika makampuni mbali mbali kufanya pesa yetu izunguke isafiri ili iweze kuongezeka pamoja na kumiliki aseti ama mali zalishi na miradi mbali mbali kama kweli tunataka kuwa na maisha bora,watoto wetu wapate elimu bora,afya bora kwa maana vyote hivyo hupatikana kwa kuwa na fedha na si vinginevyo.
Amua kuchukua hatua sasa ,kuthubutu kubadilisha maisha yako,fanya maamuzi sasa usisubirie kesho.
0765938008



No comments:

Post a Comment